Tuesday, 31 January 2017

CCM IRINGA YAZINDUA SHEREHE ZA KUADHIMISHA MIAKA 40



Na Friday Simbaya, Iringa

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu amewashukuru wazee wasisi wa chama hicho kwa kukijenga imara na misingi bora. 

Alisema kuwa CCM ina misingi bora na kinawajali wananchi, na kuongeza kuwa pasipo kuwa na wazee hao chama kisingejenga misingi imara.

Msambatavangu ambaye alikuwa mgeni rasmi alitoa kauli hiyo juzi wakati wa uzinduzi wa sherehe za kutimiza miaka 40 ya CCM zinatarajiwa kuadhimishiwa Dodoma tarehe 5 Februari mwaka huu, ambapo zitaadhimishwa kwa mikutano ya ndani na makongamano.

Mwenyekiti huyo amepongeza misingi bora iliyojenga na viongozi hao kwa kuachiana madaraka kwa utaratibu mzuri.

Akitoa mfano wa Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere kuongoza taifa hili na baadae kumuachia Mzee Mwinyi naye kumuachia Benjamin Mkapa na Mkapa kumuachia Jakaya Kikwete na kikwete kumkabidhi nchi Dkt. John Magufuli.

“Hiyo yote ni misingi bora na imara iliyojengwa na viongozi wasisi wa taifa hili. Ni bora kuenzi amani iliyopo kwa manufaa na ustawi wa nchi.,” alisema.

Aidha, Msabatavangu alionesha kukelwa na vitendo vya ubakaji kila kukicha ambapo watoto wadogo wanabakwa, jambo ambalo ametakalikema mara moja.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Mjini, Abed Kiponza amewashukuru wananchi wote wa Mkoa wa Iringa kwa uvumilivu wao wanaoonesha pamoja na kupoteza Jimbo la Iringa mjini.

Jimbo hilo kwa sasa linaloongozwa na Mchungaji Peter Msigwa kupitia CHADEMA, na kuwataka wananchi kuendelea kuwavumilia wakati huu chama kikuendelea kujiimarisha katika chaguzi zijazo.

Kiponza alisema kuwa wakati sherehe kutafanyika shughuli mbalimbali ambapo kata za Kigamboni na Kitwiru mjini Iringa zitajengwa ofisi za kata katika maeneo hayo, na tayari ujenzi unaendelea. 

Vilevile amewataka viongozi mkoani Iringa kuwahimiza wanachama katika maeneo yao na kuwakumbusha kulipa ada ya uanachama.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa mjini, Nuru Ngereja alisema kuwa katika miaka 40 ya maadhimisho, chama kimepanga kutembelea vituo vya kulelea watoto yatima ikiwepo Hospitali ya Manispaa ya Frelimo.

Hata hivyo alisema kuwa lengo la kuundwa Chama cha Mapinduzi ni kuendeleza harakati zilizokuwa zikifanywa na vyama vya ASP na TANU za kuwaletea maendeleo Watanzania kwa haraka bila ya ubaguzi wa aina yoyote nchini kwani ndivyo vyama zilivyoleta ukombozi.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amewataka wenyeviti wa CCM na kata kutoa taarifa za maendeleo ya kata ili kurandana kasi ya Magufuli ya ‘hapa kazi tu.’

Kasesela aliomba viongozi hao wanaCCM kujitahidi kuhimiza usafi wa mazingira katika maeneo yao, ili kutimiza lengo la usafi wa kila mwisho wa mwezi.


No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...