Jina la waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa limetajwa na mkazi mmoja wa Mbeya mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla kuwa sababu ya deni la shilingi milioni moja kutokana na mahaba ya wafuasi wake.
Mkazi huyo wa kata ya Ruanda Nzovwe aliyejitambulisha kwa jina la Amos Mwakyambiki alidai kuwa wafuasi wa Chadema waliharibu paa la nyumba yake walipopanda kwa lengo la kufuatilia mkutano wa Lowassa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, na kwamba chama hicho kilimuahidi kumlipa fidia ya shilingi milioni moja lakini hadi sasa ahadi hiyo haijatekelezwa.
Alimueleza mkuu wa mkoa huo kuwa kutokana na uharibifu huo mkubwa uliofanyika, wapangaji wake waliamua kuhama nyumba yake hivyo kukosa kipato.
“Naomba Serikali ya Mkoa inisaidie kuzungumza na meya (wa Chadema) ili niweze kulipwa stahiki zangu kwani sasa sijui hatma yangu. Kuku niliokuwa nauza kwa ajili ya kupata nauli kwenda ofisi za jiji wamekwisha,” Mkaazi huyo anakaririwa.
Kutokana na madai hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya alimuagiza Mkuu wa Wilaya kufuatilia suala hilo huku akitahadharisha wananchi kuhusu matumizi ya nyumba zao wakati wa kampeni.
“Lakini na nyie wananchi msikubali nyumba zenu zibadilishwe kuwa viwanja vya siasa,” alisema Makalla.
Akizungumzia taarifa hizo, Mkuu wa Idara ya Habari ya Chadema, Tumaini Makele alisema kuwa chama hicho kitafuatilia kuona ni nani aliyetoa ahadi hiyo kwa mwananchi huyo na ilikuwa katika mazingira gani ili walifanyie kazi ipasavyo.
No comments:
Post a Comment