Sunday, 26 March 2017

MANISPAA YA IRINGA YATOA MKOPO WA 70M/- KWA WANAWAKE NA VIJANA










HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa, mkoani Iringa imetoa mkopo kwa vikundi 35 vya wanawake na vijana ikiwa ni utekeleza wa agizo la serikali la kutenga asilimia kumi (10%) ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi hivyo jana.

Akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 70,000,000/- kwa vikundi hivyo katika awamu ya pili ya kipindi cha mwaka 2016/2017, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Alex Kimbe amewataka kinamama na vijana kutumia fedha hizo kwa shughuli zilizokusudiwa ili ziweze kuleta manufaa na kuwatoa katika lindi la umasikini.

Alisema kuwa jumla ya vikundi 35 toka katika kata zote 18 za Manispaa ya Iringa vimepokea mikopo, ambapo vikundi 16 vya vijana vimepokea jumla ya shilingi milioni 32,000,000/- na shilingi milioni 38,000,000/- zimetolewa kwa vikundi 19 vya wanawake.

Kimbe alisema mkopo huo umetolewa kwa awamu ya pili, ambapo kwa awamu ya kwanza kipindi cha mwaka 2016/2017 Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ilitoa kiasi cha shilingi milioni 70,147,000/- kutoka mapato ya ndani kwa vikundi 35 vya wanawake na vijana.

Aidha, jumla ya 647,000/- zilitumika kwa ajili ya kuwajengea uwezo viongozi wa vikundi vilivyokopeshwa, ambapo vikundi 18 vya vijana na vikundi 17 vya wanawake vilinufaika.

Naye Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Iringa, Eliah Kasanga alisema kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na watendaji wa kata wameendelea kufanya ufautiaji kwa vikundi vilivyokopeshwa, na mpaka Januari, 2017 jumla ya 39,788,000/- zimerejeshwa na ufualiaji unaendelea.

Alisema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imekuwa ikitekeleza agizo la serikali la kutenga asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana.

Kasanga aliongeza kuwa agizo hilo lilianza kutekelezwa kuanzia mwaka 2012 kwa kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake tu na kufikia mwaka 2013 mikopo hiyo ilianza kutolewa kwa vikundi vya vijana pia.

Alisema kuanzia mwaka 2012/2013 mpaka 2016/2017 kiasi cha shilingi 175,100,000/- zimenufaisha walengwa 1,243 wa vikundi vya wanawake na vijana.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mikopo ya Vijana Manispaa ya Iringa, Maria Sangana alisema mfuko huo umekuwa ukikabiriwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na vikundi kutorejesha fedha walizokopeshwa kwa wakati.

Alisema kuwa hali hii imekuwa ikichelewesha utoaji wa mikopo kwa vikundi vingine na kuongeza kuwa baadhi ya vikundi kutotumia fedha kwa shughuli walizopanga wakati wa kuomba mkopo.

Pia, Sangana alisema kuwa baadhi ya vikundi vinakabiliwa na mikopo mengine mingi toka taasisi zingine za fedha na kuongeza kuwa kuna upotoshaji unaendelea mitaani kuwa fedha inayotolewa na serikali ni msaada.


Aidha, katika kukabiliana na changamoto hizo ofisi ya maendeleo ya jamii katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeeandaa mfumo wa ufuatilaji wa marejesho ya fedha za mfuko huo, pamoja na kuendelea kutoa elimu ya stadi za kazi na ujasiliamali kwa kivundi vya ujasiliamali.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...