Sunday, 26 March 2017

ZAIDI YA 80 IRINGA WAPATA MAFUNZO YA UKARIMU NA UTALII


Mwenyekiti wa vikundi vya asili vya ngoma kutoka Ikwavila New Force katika Kijiji cha Mahuninga, tarafa ya Idodi wilayani Iringa, mkoani Iringa, Recktika Palinoo (wa mbele kulia) pamoja na katibu wake Leonatus Kikoti wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza (hayupo pichani) wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya ukarimu na utalii yaliyofanyika mkoani Iringa jana.  (Picha na Friday Simbaya)


MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amewataka watoa huduma katika sekta ya ukarimu na utalii kanda ya kusini kuboresha huduma zao ili kukidhi haja soko la utalii katika ukanda huu.

Alisema kuwa ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za taifa za kusini watoa huduma kwa kushirikiana na sekta binafsi hawanabudi kuinua viwango vya utowaji wa huduma.

Masenza alisema hayo wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa watoa huduma katika sekta ya ukarimu na utalii yaliyofanyika mkoani Iringa jana.

Alisema kuwa serikali ipo katika machakato wa kuboresha miundombinu za barabara na viwanja vya ndege ili kurahisha watalii kufika katika hifadhi pamoja na vivutio vilivyopo katka ukanda wa kusini.

Alisema kuwa takwimu za mwaka 2015 zinaonesha kuwa watalii wengi zaidi walitembelea mbuga za kanda za kaskazini kuliko kanda ya kusini, kwa hiyo mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuboresha utoaji wa huduma katika kanda ya kusini.

Zaidi wa washiriki wa 80 wamepata mafunzo ya ukarimu na utalii yaliaanza tarehe 22 hadi 24 Machi mwaka huu, yaliyotolewa na Chuo cha kitaifa cha utalii kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na SPANEST kwa ufadhili shirika la umoja wa mataifa la maendeleo (UNDP).

Alisema mafunzo hayo wamewaongezia ujuzi pamoja na kujiamini wakati wa kutoa huduma kwa watalii wanaotembelea ya kanda ya kusini.

Aidha, Masenza alisema Wizara ya Maliasili na Utalii ipo katika mchakato wa kutunga kanuni zitakazowazuia wafanyakazi wa hoteli wasio na vyeti vinavyotambulika na serikali kutoa huduma katika sekta ya utalii.

Alisema kuwa kanuni hiyo ambayo msingi wake unalenga kuendeleza na kuboresha huduma katika ya sekta hiyo, utahusisha pia kuvibana vyuo vya hoteli na utalii ili vitoe mafunzo yanayokidhi viwango.

“Baada ya kutungwa na kuanza kutumika kwa kanuni hizo, waajiri katika sekta hiyo watalazimika kuwaajiri wafanyakazi wenye sifa ambao wamesajiliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii,” alisema Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utalii, alisema Masenza.

Aliyasema hayo jana kwenye mafunzo ya siku tatu ya ukarimu na utalii yanayoshirikisha watoa huduma zaidi ya 80 wanaofanya biashara inayohudumia watalii mkoani Iringa.

Mafunzo hayo yanayotolewa na wizara hiyo kwa kushirikiana na Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST), yanafanyika kwa siku tatu mjini Iringa.

Masenza alisema mafunzo hayo ya muda mfupi yameanza kutolewa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini baada ya serikali kubaini baadhi ya vyuo vinavyotoa mafunzo hayo kuyatoa chini ya viwango.

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki alisema changamoto hizo zimesababisha huduma duni katika maeneo ya mapokezi, chakula, vinywaji na malazi, na hivyo kuleta malalamiko makubwa sana kwa wageni.





Kwa kupitia mafunzo hayo mafupi Meing’ataki alisema; “ni mtarajio yetu maarifa watakayopata washiriki hawa yatawawezesha kutambua wajibu wao ili wageni wanaopata wapate huduma wanazotarajia.”

“Sekta ya utalii ina changamoto nyingi, lakini eneo hili la huduma ni muhimu kwasababu linaweza kusaidia kumrudisha mgeni tena na tena na kumfanya awe balozi kwa watu wengine,” alisema.

Kwa wawekezaji katika sekta hiyo, haitoshi tu kuwa na hoteli kubwa kama itakuwa haina huduma bora kwa wageni wake.

Awali, akifungua mafunzo hayo tarehe 22 Machi, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Fikira Kissimba alisema licha ya ukanda wa nyanda za juu kusini kuwa na vivutio vingi vya utalii, idadi ya watalii wanaovitembelea ni ndogo na moja ya sababu yake ni uduni wa huduma katika sekta hiyo ya utalii.


Akishukuru wizara ya maliasili na utalii na SPANEST kwa kutoa mafunzo hayo, Kissimba alisema yatakuwa chachu katika kukuza na kuendeleza utalii kusini mwa Tanzania kwa kutoa huduma bora kwa watalii.

Aliwataka wahudumu katika sekta hiyo waache tabia ya uvivu, kufanyakazi kwa mazoea na wawe wepesi kujifunza ili kuboresha huduma zao.



No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...