Sunday, 21 May 2017

Watumishi Sita Manispaa Ya Iringa Wafukuzwa Kazi Kwa Utoro


Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Alex Kimbe akifungua kikao cha baraza la madiwani cha robo ya tatu ya mwaka 2016/2017 wa halmashauri hiyo leo unaofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Iringa jana. (Picha na Friday Simbaya)


Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Alex Kimbe akimkabidhi mmoja ya watumishi wa halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Musa Mwaihojo (kulia) cheti cha pongezi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri hiyo, ikiwa ni pamoja na ushuru wa mabango na leseni wakati wa kikao cha baraza la madiwani cha robo ya tatu ya mwaka 2016/2017 wa halmashauri hiyo leo unaofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Iringa jana. (Picha na Friday Simbaya)


BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, mkoani Iringa limewafukuza kazi watumishi wake sita na kumrudisha kazini mmoja kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo utoro kazini.

Meya wa Manispaa ya Iringa Alex Kimbe, ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza la madiwani aliwataja watumishi hao waliokumbwa na adhabu hiyo kwa utoro kazini kuwa ni Glory Ngowi, Anzawe Mvena, Francis Mtenge, Paul Sanga, Mkombozi Gendagenda na Tumaini Sanga.

Kimbe alikiambia kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Manispaa ya Iringa jana (Jumamosi) kuwa watumishi hao sita (6) wamefukuzwa kazi kutokana na kutokuwepo kwenye vituo vyao vya kazi bila taarifa yoyote.

“Watumishi hawakuwepo kazini kwa zaidi ya miaka miwili na wamefukuzwa kutokana na kutokuwepo kazini kwa zaidi ya miaka miwili bila ruhusa ya mwajiri wake kinyume na Kanuni za Utumishi wa umma za mwaka 2003, na kuanzia leo tarehe 20 mwezi Mei, mwaka 2017 watajwa hapo juu sio watumishi wa halmashauri ya Manispaa ya Iringa,” alisema Kimbe.

Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani huyo alisema kuwa halmashauri hiyo imemrudisha kazini Lucy Mtafwa baada ya kamati kuridhia kuwa hakutenda makosa ya kiutumishi na hatimaye baraza lilipendekeza mtumishi huyo arudishwe kazini. 

Wakati huo huo, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imekusanya zaidi ya shilingi milioni 400 (400m/-) kodi ya mapato kwa mwezi Machi mwaka 2017.

Meya wa Manispaa ya Iringa Alex Kimbe kwa kutambua mchango wa usimamizi wa ukusanyaji kodi aliwatunuku vyeti vya pongezi vya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri baadhi ya watumishi waliosimamia zoezi hilo.

Akiongea wakati wa kikao cha baraza la madiwani cha robo ya tatu ya mwaka 2016/2017, meya huyo alisema mapato hayo ni kutokana na ushuru wa mabango na leseni.

Kikao cha baraza la madiwani halmashauri ya Manispaa ya Iringa cha robo ya tatu ya mwaka 2016/2017, kilikaa na kujadili taarifa mbalimbali za miradi ya maendeleo pamoja kuwafukuza kazi watumishi sita kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo utoro kazinina kumrudhi mmoja kazini.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...