SIKU Moja baada ya Ofisi za IMMMA Advocates zinazomilikiwa na Mawakili Fatma Karume na Lawrence Masha kuungua kwa shambulio la mlipuko wa Mabomu,Rais wa chama cha Mawakili Tanganyika Tundu Antiphas Lissu, amewataka mawakili wote nchini kutokwenda mahakamani siku ya jumanne na jumatano, kuonyesha kupinga vitendo walivyofanyiwa mawakili wenzao wa IMMMA, ambao ofisi yao ilichomwa moto.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo hii, Tundu Lissu amesema kitendo hicho kinaingilia uhuru wa wanasheria na taaluma ya sheria, kinahatarisha uhuru wa mahakama na utawala wa sheria kwa ujumla, na kuwataka mawakili walio nchini Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kutoonekana mahakamani kufanya kazi yao.
"Baraza la uongozi linawataka wanachama wa TLS nchi nzima kususia kuhudhuria katika mahakama pamoja na mabaraza ya aina zote kati ya siku za jumanne na jumatano ya tar 29 na 30 Agosti 2017, kwa lengo la kuwaunga mkono mawakili wa IMMMA, na kuonyesha kutokukubaliana kwetu na vitendo vya kihalifu vya kuwashambulia mawakili hao kwa mabomu", alisema Tundu Lissu.
Tundu Lissu aliendelea kusema ..."Mawakili wa IMMMA wameshambuliwa ofisi zao zimepigwa mabomu, nyaraka zimepotea zingine zimeungua moto, hawataweza kwenda mahakamani kwa sababu vitendea kazi vyao vimeharibiwa, sisi mawakili wengine wote nchi nzima, tuna wajibu wa kuwaunga mkono mawakili wa IMMMA kwa kutoenda mahakamani vile vile, akiumizwa mmoja tumeumizwa wote, kwa hiyo tunawataka wanachama wetu popote walipo kesho kutwa wasiende mahakamni, wasiende kwenye mabaraza yoyote ili kuwaunga mkono wenzetu ambao wameshambuliwa", alisema Tundu Lissu.
Ofisi ya za mawakili wa IMMMA zilizopo Upanga jijini Dar es Salaam zimeungua moto usiku wa Ijumaa, na mpaka sasa waliohusika na tukio hilo bado hawajafahamika.
No comments:
Post a Comment