Wednesday, 30 August 2017

WANANCHI KILOLO WAASWA KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA KUPANGA MIPANGO





Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la “The Mazombe Mahenge Development Association” (MMADEA) la mkoani Iringa, Raphael Mtitu akitambulisha mradi wa ushiriki wa wananchi katika kupanga mipango ya maendeleo ya vijiji kwa Kamati ya Uongozi ya Wilaya (CMT) katika Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa juzi. (Picha na Friday Simbaya)


MKURUGENZI wa shirika lisilo la kiserikali la “The Mazombe Mahenge Development Association” (MMADEA) la mkoani Iringa, Raphael Mtitu amesema ili kuwa na maendeleo endelevu katika jamii ni lazima miradi ishirikishe jamii katika mifumo ya upangaji mipango na bajeti katika setka mbalimbali kwa kutumia dhana ya fursa na vikwazo kwa maendeleo (O&OD).

Alisema kuwa ili miradi iweze kuwa endelevu ni lazima ishirikishe jamii katika kupanga mipango ili kuweza kuwa na matokeo bora na hatimaye kutekeleza malengo yaliyotarajiwa.

Mtitu alisema hayo Ijumaa ya wiki iliyopita wakati kitambulisha mradi wa ushiriki wa wananchi katika kupanga mipango ya maendeleo ya vijiji kwa Kamati ya Uongozi ya Wilaya (CMT) katika Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.

Alisema kuwa miradi mingi inayoibuliwa kwa niaba ya wananchi inashindwa kuendelea, kumbe miradi hiyo ingeikuibuliwa na wananchi wenyewe na kuimilikishwa itatoa matokeo chanya.

Mradi huo wa ushiriki wa wananchi katika kupanga mipango ya maendeleo ya vijiji utatekelezwa katika kata nne na vijiji 13, ambao unatarajia kuwa miaka miwili (2) kuanzia Agosti 2017 hadi Disemba 2018 na unatarajia kugharimu shilingi milioni mia moja sitini (160,000,000/-), kuwa ufadhili kutoka kwa “The Foundation for Civil Society” (FCS) .

Alisema kuwa watatekeleza mradi katika kata za Idete katika vijiji vya Idete, Madege na Kiwalamo, Kata ya Ibumu katika vijiji vya Ilambo, Kilalakidewa, Kilumbwa na Ibumu, Kata ya Uhambingeto katika vijiji vya Uhambingeto, Kipaduka na Ikuka na Kata ya Nyanzwa katika vijiji vya Igunda, Nyanzwa na Mgowelo.

“Lengo la mradi ni kuishirikisha jamii katika mifumo ya upangaji mipango na bajeti katika sekta mbalimbali kwa kutumia fursa na vikwazo kwa maendeleo (O&OD),” alisema Mtitu.

Alisema kuwa mmoja ya malengo mahususi ya mradi ni kuongeza ushiriki wa jamii katika upatikanaji wa taarifa katika mchakato shirikishi jamii wa upangaji mipango na bajeti za idara mbalimbali kama vile kilimo, elimu na maji.

Aidha, mkurugenzi huyo wa MMADEA alisema kuwa shughuli zitakazo tekelezwa kwa robo ya kwanza (mwezi 8 hadi 10/2017) ni kama zifuatazo;

Kufanya utambulisho wa mradi kwa halmashauri ya wilaya na wadau wa maendeleo ili kupata maoni na ushauri kuhusu mradi huo.

Kufanya uhamasishaji kwa viongozi 390 ili waone umuhimu wa kushirikisha wananchi katika kuibua na kupanga vipaumbele vyao kwa kutumia dhana ya fursa na vikwazo kwa maendeleo (O&OD).

Pamoja na kuendesha mikutano ya hadhara kwa wananchi 1040 ili waweze kuona umuhimu wa wao wa kushiriki kikamilifu katika kuibua na kupanga vipaumbele vyao ili viingizwe kwenye mpango wa maendeleo ya vijiji.

Awali, akitoa salama za serikali wakati kikao cha kitambulisha mradi wa ushiriki wa wananchi katika kupanga mipango ya maendeleo ya vijiji, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilolo (DAS), Yusufu Msawaga alilipongeza shirika la MMADEA kwa kuleta mradi huo kwa halmashauri yao.

DAS huyo aliwaagiza viongozi mbalimbali wa halimashauri hiyo pamoja na madiwani ambao mradi huo utatekelezwa katika maeneo yao kutoa ushirikiano pamoja na kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu.

Kwa upande wao, Diwani wa Kata ya Idete, Bruno Hakimu Kauku na Diwani wa Kata Uhambingeto, Tulinumtwa Alfons Mlangwa kwa pamoja walisema kuwa mradi huo umekuja wakati mwafaka kwa vile utasaidia wananchi katika kuibua miradi yao kuanzia ngazi ya kitongoji hadi kijiji.

Walisema kuwa mradi huo pia utaongeza ushiriki wa jamii katika kupanga mipango na bajeti kupitia dhana ya O&OD, pamoja na wananchi kudai uwajibikaji katika utekelezaji.


No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...