Thursday, 16 November 2017

MBOWE AWATAKA KITWIRU KUFUNGUA VYUMA KWA KUINYIMA KURA CCM























MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amewataka wapiga kura wa kata ya Kitwiru, Mjini Iringa kupeleka ujumbe wa hali ngumu ya maisha kwa Rais Dk John Magufuli kwa kumchagua mgombea wa chama chake kuwa diwani wa kata hiyo.


“Wakati wananchi wakilalamika vyuma vimekaza, watu hawana hela mifukoni, manunuzi yanapungua na baadhi ya biashara ndogo, za kati na za wawezekazaji wakubwa zikifungwa, kuna baadhi ya madiwani wa upinzani wananuliwa kwa kati ya Sh Milioni 2 na Milioni 5 halafu hela za kodi zinazolipwa na watanzania masikini zinatumika kuitisha chaguzi ndogo kwa gharama kubwa,” alisema.


Mbowe alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikitumia hadi Sh Milioni 200 kugharamia uchaguzi wa kata moja ambayo diwani aliyekuwepo ananunuliwa kwa Sh Milioni 5.


Akizungumzia hali ya maisha ya mtanzania kwasasa Mbowe aliwauliza mamia ya wanachi waliojitokeza katika mkutano wa kampeni uliomnadi mgombea wao udiwani wa kata hiyo Bahati Chengula tofauti ya kipato na hali ya maisha wanavyoina sasa na wakati wa utawala wa Jakaya Kikwete; wote walinyosha vidole wakiashiria wakati wa Kikwete hali ya maisha ilikuwa na nafuu.


Katika mkutano huo Mbowe alizungumzia pia masuala mbalimbali ikiwemo deni la Taifa akisema kwa sasa kila mtanzania wakiwemo watoto wachanga anadaiwa wastani wa Sh Milioni 1.2.


Akazungumzia pia hali ya kisiasa na jinsi wanasiasa wanavyozuiwa kufanya mikutano, kusitishwa taarifa za moja kwa moja za bunge, shambulio dhidi ya Mbunge Tundu Lissu, na jinsi chama hicho kilivyompokea kwa mikono miwili, Lazaro Nyalandu.


Akiomba kura, mgombea wa udiwani wa kata hiyo aliwaomba wapiga kura wa kata hiyo wamchague kuwa diwani wao ili akaungane na madiwani wanaounda halmashauri ya manispaa ya Iringa kupitia chama chake hicho kushughulikia changamoto mbalimbali za kimaendeleo.


"Nayafahamu matatizo ya kata hii katika sekta zote ikiwemo ya afya, elimu, miundombinu ya barabara, maji, maeneo ya biashara na mengine mengi, Nipeni kura nikawatumikie," alisema.


Naye Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amesema anaingiza miguu yote katika kampeni za kata hiyo kuanzia kesho.


"Vikao vya bunge vinamalizika kesho, siendi tena bungeni, siku kumi zote zilizobaki nitabanana katika kata hii hadi kieleweke," alisema. 

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...