Na Friday Simbaya, Iringa
MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amepongeza Mradi wa NAFAKA kwa juhudi za kuinua uchumi wa vikundi vya wakulima na kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo.
Alisema kuwa Kilimo kinatoa mchango mkubwa wa ajira kwa vijana na wanawake walioko vijijini na mijini kwa maendeleo yetu na Taifa kwa ujumla.
Masenza alisema hayo jana wakati wa kukabidhi zana za kilimo kwa wakulima katika vikundi vya uzalishaji, na kuongeza kuwa zana hizo za kilimo zitasaidia wakulima kuongeza tija, uzalisahji na kufanya shughuli za kilimo kwa wakati.
Pia, alisema kuwa nyenzo hizo za kilimo zitawezesha vijana na wanawake kushiriki katika kilimo kwa mafanikio makubwa ikiwa pamoja na kukuza uchumi wa kipato katika ngazi ya kaya pamoja na kupunguza umasikini kwenye mkoa wa Iringa.
“Serikali inahimiza sana wakulima wadogowadogo, wakulima wakati na wakubwa kutumia zana bora za kilimo katika shughuli za uzalishaji mazao ili kuongeza tija na maeneo ya mashamba yanayolimwa na zana bora za kilimo,” alisema Masenza.
Masenza alisema kuwa Mpango wa Ruzuku wa Zana za Kilimo unaotolewa na Mradi wa NAFAKA wa USAID, ni fursa muhimu kwa Vikundi vya wakulima.
Pia serikali itaendelea kuwaunganisha wakulima na vikundi vya wakulima kwenye fursa mbalimbali ambazo zinapatikana serikalini ikiwa ni juhudi za kuunga mkono Serikali ya Awamu ya tano (5) katika kuimarisha kilimo na kuongeza thamani ya mazao kwa kukoboa na kusanga badala ya kuuza kama nafaka au mali ghafi.
Kwa upande wake, Meneja Ruzuku wa Mradi wa NAFAKA wa USAID, Pius Tizeba alisema kuwa mradi umetoa ruzuku ya zana za kilimo yenye jumla ya thamani ya Tsh. 303,497,000/- kati ya hizo vikundi vya wakulima vimechangia jumla ya Tsh. 52,252,000/-.
Aidha vikundi tisa (9) kutoka wilaya za Kilolo na iringa vimepata ruzuku ya zana za kilimo yenye thamani ya Tsh. 74,930,000/-, ambapo vikundi vimechangia jumla ya Tsh. 9,938,000/-.
Tizeba alisema zana za kilimo ambazo vikundi vya wakulima toka wilaya za Kilolo na Iringa walikabidhiwa ‘Power Tiller’ nne (4) zenye thamani ya Tsh. 36,400,000/-,mashine za kukoboa na kusaga mahindi tatu (3) zenye thamani ya Tsh. 24,450,000/- na vifaa vya kinga wakati wa kupuliza viuatilifu mashambani vyenye thamani ya Tsh. 14,080,000/-.
Alisema kuwa pamoja na mafanikio ya vikundi vya wakulima kuweza kuchangia ruzuku kwa kupata za za kilimo, wanakabiliwa na changamoto za kukosa fedha za kujengea jengo la kuweka mashine za kusaga na kukoboa pamoja na kuunganisha umeme,kutokuwa na ujuzi wa kulima kwa kutumia ‘power tiller’.
No comments:
Post a Comment