Tuesday, 27 February 2018

RC Masenza Awataka Wakandarasi Kufanya Kazi Kwa Ufanisi Na Viwango Vya Ubora







Mratibu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Iringa Iringa Eng Juma Wambura (wa pili kulia) akimkabidhi mmoja wakandarasi mkataba (Picha na Friday Simbaya)







IRINGA: Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amewataka wakandarasi wote walioshinda zabuni kufanya kazi kwa kuzingatia muda uliopangwa na viwango vya ubora wa kazi. 

Alisema kuwa Serikali haitamvumilia mkandarasi yeyote atakayefanya kazi chini ya muda uliopangwa kwenye Mkataba, Lakini pia haitamvumilia Mkandarasi atakayefanya kazi chini ya viwango. 

RC Masenza alisema hayo jana wakati akishuhudia hafla fupi ya kutiliana saini mikataba ya miradi ya ujenzi wa barabara kati ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Iringa na wakandarasi walioshinda zabuni kwa mwaka wa fedha 2017/2018. 

Alisema kuwa katika kuhakikisha ufanisi wa kazi na ubora unaotakiwa, Serikali imeajiri Mameneja wa TARURA katika kila halmashauri. 

“Jukumu kubwa la Mameneja hawa ni kuwasimamia wakandarasi ili watekeleze wajibu wao. Hivyo, Mameneja wa Halmashauri pia mjipange sawasawa kuhakikisha ubora na thamani ya fedha inapatikana,” alisema. 

Alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya malipo kwa wakandarasi na changamoto nyingi zimekuwa zikisababishwa na uzembe na kutokufuata taratibu. 

Masenza alisema anamatumaini kuwa wakandarasi hawa watalipwa kwa wakati baada ya kuwa wametimiza wajibu wao, wamefikia vigezo vya ubora kwa mujibu wa mikataba, na kuongeza kuwa utekelezaji huo utawafanya kuongeza morari ya kazi na pia kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima kwa Serikali. 

“Namuagiza Mratibu wa TARURA Mkoa kusimamia na kuratibu shughuli zote za ujenzi na ukarabati ikiwa ni pamoja na kuwasimamia Mameneja wa TARURA wa Halmashauri kutekeleza majukumu yao na Wakandarasi kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Mikataba,” alisema. 

Lakini pia alimtaka Mratibu wa TARURA Mkoa kuweka utaratibu mzuri utakaowaripoti Wakandarasi watakaoshindwa kwenda na kasi ya serikali ya awamu ya tano ya Rais, Dr. John Magufuli na watakaofanya kazi kwa kulipua ili taarifa zao ziwasilishwe kwa mamlaka husika na hatimaye waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi na ikiwezekana wasipewe tena kazi za ujenzi. 

“Nichukue nafasi hii tena kuwapongeza wakandarasi walioshinda zabuni za ujenzi na kusaini mikataba ya ujenzi wa barabara kwa mwaka wa fedha 2017/2018 katika mkoa wa Iringa. Natumaini uzalendo kwa nchi utawekwa mbele kwa maslahi mapana ya Tanzania na maendeleo ya nchi yetu,” alisema RC Masenza. 

Kwa upande wake, Mratibu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Iringa Iringa Eng Juma Wambura alisema kuwa mikataba kati ya wakandarasi walioshinda zabuni na TARURA ya Miradi ya Barabara kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni kuwa gharama ya shilingi za kitanzania bilioni 3.56. 

Eng. Wambura alisema kuwa TARURA imechukua majukumu ya kiutendaji kuhusiana na ujenzi na matengenezo ya mtandao wa barabara za vijijini na mijini ambayo yalikuwa yakitekelezwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM) na kuratibiwa na Kurugenzi ya Miundombinu chini ya Wizara OR- TAMISEMI. 

Alisema kuwa Kuanzishwa kwa TARURA kunatenganisha majukumu ya kiutekelezaji na yale ya usimamizi na TARURA inategemewa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya ki-biashara, ufanisi wa gharama (Cost Effectiveness), masuala mtambuka (mazingira, usalama, na masuala ya kijamii) kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kijamii na ki-uchumi. 

Alisema kuwa TARURA Mkoa wa Iringa inahudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya Kilomita 4601.25 inayojumuisha Halmashuri tano ambazo ni Iringa Manispaa, Halmashauri za wilaya za Iringa, Kilolo, Mufindi na Mji wa Mafinga. 

“TARURA Mkoa wa Iringa ilitangaza miradi ya barabara ya halmashauri zote za Mkoa, jumla ya Zabuni 26 yenye thamani ya Tsh 6.5 bilioni ambayo leo utaishuhudia Mikataba 18 ikisainiwa na Wazabuni walioshinda baada ya mchakato mzima wa manunuzi kukamilika yenye thamani ya Tsh 3.56 bilioni,” alisema Eng. Wambaura. 


No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...