Meneja Selebu Rocks Spring Water Ltd Edgar Lamba (kulia) akikabidhi msaada wa vifaa vya umeme jua (solar panel kits) kwa Paroko Fr. Silvanus Ndazi wa Parokia ya Mtandika, Jimbo Katoliki Iringa jana.
KILOLO: Parokia ya Mtandika katika Jimbo Katoliki Iringa wilayani Kilolo mkoani Iringa itasherehekea Siku Kuu ya Pasaka kwa mwanga baada ya kupata msaada wa umeme wa nishati ya jua (solar panel kits) kutoka Selebu Rocks Spring Water Ltd Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.
Msaada huo wenye thamani shilingi milioni 6.9 ni mchango kutoka kwa mkurugenzi na mfanyabiashara mkongwe Mzee John Lamba wa Kiwanda cha maji wilayani kilolo, mkoani Iringa.
Akizungumza jana wakati wa kukabidhi vifaa hivyo vya umeme wa jua, Meneja Selebu Rocks Spring Water Ltd Edgar Lamba kwa niaba ya mkurugenzi na mfanyabiashara mkongwe Mzee John Lamba alisema kuwa wamesukumwa kutoa vifaa hivyo ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za kiroho nyakati zote na kuzingatia kuwa Parokia ya Mtandika haijafikiwa na umeme wa Gridi ya Taifa.
“Parokia ya Mtandika inakabiliwa na changamoto ya umeme kwa muda mrefu sasa…,” alisema meneja huyo.
Alisema kuwa kampuni hiyo imetoa msaada wa nishati ya umeme wa jua ili waumini wa parokia hiyo pamoja na mapadre washerehekee Siku Kuu ya Pasaka kwa mwanga.
Lamba aliongeza kuwa Parokia ya Mtandika ipo mbali na gridi ya umeme wa Taifa hivyo kukosa huduma hiyo muhimu ya umeme na kuongeza kuwa umeme huo utawekwa pia katika nyumba ya mapadri.
Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya Parokia ya Mtandika Paroko Fr. Silvanus Ndazi alishukuru kwa msaada huo wa nishati ya umeme ya jua na kuongeza kuwa waumini wa parokia hiyo watasherekea siku kuu ya Pasaka kwa mwanga wa uhakika.
Alisema kuwa parokia nyingi zilizopo maeneo ya vijijini ambazo hazijafikiwa na umeme wa gridi ya Taifa zimekuwa zinasherekea siku kuu wakati wa usiku kwa kutumia vibatari, taa na tochi jambo ambalo limekua linahatarisha usalama.
“Lakini leo tumepata ufumbuzi wa mwanga kwa hiyo waumini watasherekea Siku Kuu ya Pasaka ambayo ni siku maalum ya kumbukumbu ya kufufuka kwa Yesu Kristo,” alisema Fr. Salvanus.
Jimbo la Katoliki Iringa lipo chini ya Askofu wa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa ambaye pia Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).Na Friday Simbaya, Kilolo
No comments:
Post a Comment