Grace Gwamagobe-Songwe
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa amesema atahakikisha anasimamia kwa ukaribu fedha zilizotolewa na serikali Mkoani hapa kwa ajili ya upanuzi wa vituo vya afya ili zifanye kazi zaidi ya ile iliyopangwa awali kutokana na kuongezeka kwa nguvu za wananchi.
Gallawa ameyasema hayo mapema jana wakati wa ziara yake Wilaya ya Mbozi alipokagua maendeleo ya upanuzi wa vituo vya afya vya Isansa kilichopokea milioni 500 na kituo cha Afya cha Iyula Kilichopokea milioni 400, kwa ajili ya ujenzi wa maabara, nyumba ya daktari, chumba cha upasuaji, jengo la mama na mtoto na chumba cha kuhifadhia maiti.
“Fedha hizi lazima zifanye kazi iliyopangwa vizuri na pia tuongeze kazi nyingine ya ziada kutokana na kuwa tumepata nguvu ya wananchi lakini pia mafundi wetu hawa tunaowatumia ni wazawa na wenyeji wa maeneo ya kwetu kwahiyo gharama zao zitatupa unafuu ambao tunatakiwa kuutumia kuongeza kazi nyingine”, amesema Gallawa.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa akizungumza na baadhi ya watendaji na wananchi wa kijiji cha Iyula waliojitokeza katika eneo la ujenzi katika kituo cha Afya cha Iyula Wilaya ya Mbozi, kituo hicho cha Afya kimepokea shilingi milioni 400 kwa ajili ya upanuzi wa kituo hicho.
|
Ameongeza kuwa licha ya upanuzi wa vituo vya afya kuchelewa kuanza bado ana Imani kuwa wataweza kumaliza ndani ya muda uliopangwa kutokana na uchapakazi wa mafundi wazawa wa maeneo hayo.
Gallawa amesema kukamilika upanuzi wa vituo hivyo vya afya kutavifanya vituo hivyo vivutie na hata mgonjwa akifika apate matumaini ya kupona na sio kukatishwa tamaa na hali mbovu ya mazingira.
“Tiba ya kwanza ya mgonjwa akifika kituo cha afya akute mazingira yanavutia na sio majengo mabovu na uchafu hivyo vitamfanya akate tamaa ya kupata matibabu sahihi, tukimaliza ujenzi wa hayo majengo tutahakikisha tunapaka rangi paa za majengo yote zifanane ili vituo vyetu vya afya vivutie”, amefafanua Gallawa.
Aidha Gallawa amemtaka Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Lauteri Kanoni kuhakikisha anaweka mfumo wa maji safi katika vituo hivyo hasa mfumo wa kuvuna maji ya mvua ili vituo vikikamilika maji yawepo kwa ajili ya matumizi.
Naye Mkazi wa kijiji cha Isansa Wilaya ya Mbozi Bi Stela Mkeya ameonyeshwa kufurahishwa na upanuzi wa kituo cha Afya Isansa huku akieleza baadhi ya kero walizokuwa wakizipata awali.
“Tunaishukuru sana serikali ya Magufuli kwakweli wametusaidia, tulikuwa tunapata shida kufuata huduma za upasuaji wa akina mama wajawazito huko hospitali ya Wilaya iliyopo Vwawa lakini pia hapa kwenye kituo cha afya mzazi akijifungua hata mazingira ya kwenda kujisafisha vizuri kama vile mabafu yakiwa hayatoshi kabisa”, ameeleza Bi Mkeya.
Kwa upande wao mafundi waliokabidhiwa kazi ya upanuzi wa vituo hivyo vya Afya wameonyesha ari ya kufanya kazi hiyo kwa ufanisi na haraka huku wakimuomba Mkuu wa Mkoa Chiku Gallawa awasaidie upatikanaji wa taa ili waweze kufanya kazi mchana na usiku naye Mkuu wa Mkoa amekubaliana na mapendekezo hayo.
MAELEZO YA Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa akizungumza na mafundi wanaojenga katika kituo cha Afya Isansa Wilaya ya Mbozi, kituo hicho cha Afya kimepokea shilingi milioni 500 kwa ajili ya upanuzi wa kituo hicho.
No comments:
Post a Comment