Na Friday Simbaya, Iringa
Waumini wa Kiislamu nchini wamehaswa kuzingatia maadili kwa kufanya matendo mema katika jamii, kwa kipindi chote watakachokuwa kwenye funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na baada ya kuisha kwa mwezi huo.
Sheikh wa Mkoa wa Iringa Abubakari Chalamila alitoa kauli wakati wa futari ilioandaliwa na Baraza la Waislamu Tanzania (BWAKATA) na kuhudhuriwa na walikwa zaidi ya 350 mjini Iringa jana.
Alisema kuwa Uislam ni dini ya amani hivyo ili mja aweze kuwa karibu na Muumba wake anatakiwa kuzidisha ibada na kufanya mambo yaliyo mema hasa kwenye mwezi wa Ramadhani.
“Mwezi wa funga wa Ramadhani tunatakiwa kufanya ibada na kutekeleza funga kama inavyotakiwa, tunatakiwa kuzidisha ibada, tuwe na subira, utiifu, nidhamu pamoja na kuzidisha imani yetu kwa muda wote,” alisema Sheikh Chamilala.
sheikh alieleza kuwa, watu wengi wamekuwa wakivutiwa na mambo yanayopoteza wakati na yasiyo na mazingatio wala manufaa katika maisha yao, hali ya kuwa wakiacha kufanya matendo mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu.
“Kuna mazingatio makubwa yanayopatikana ndani ya Mwezi Mtukufu, kama kuongeza imani zetu na kupata faradhi mbalimbali zitakazoongeza swawabu kwa matendo tunayoyafanya,” aliongeza.
Sheikh Chalamila aliongezea kuwa “Watu wanatakiwa kujikita zaidi kwenye ibada, kwani tunafunga mwezi kwa mwaka tena ni siku chache hivyo watu wanatakiwa kuwa wavumilivu ni kipindi kifupi cha mpito, lakini utakuta watu wanaingia uvivu hatimaye mwezi unaisha bila ya kufanya ibada zozote muhimu.”
No comments:
Post a Comment