Iringa — Shamrashamra na tambo za soka zimechukua nafasi
leo katika mtaa wa Mantigo, kata ya Miyomboni,
Manispaa ya Iringa, baada ya mashabiki wa timu hasimu za Simba SC
na Yanga SC kukutana na kushindana kwa kauli kuelekea pambano
la watani wa jadi litakalohusisha pia Ngao ya Jamii, kuashiria
mwanzo wa msimu mpya wa Ligi Kuu NBC Tanzania Bara 2025/2026.
Mashabiki hao walisisitiza kuwa mechi hiyo itakuwa kivutio kikubwa si tu kwa
wakazi wa Iringa, bali pia wageni kutoka mikoa jirani, huku kila upande
ukijiamini kutwaa ushindi na kutoa taswira ya mwelekeo wa msimu mpya.
“Msimu huu Simba haiwezi kufungwa, tunakuja kuchukua alama tatu muhimu
Iringa,” alisema kwa kujiamini David Bovansi, shabiki
kindakindaki wa Simba SC.
Upande wa Yanga nao ulijibu mapigo.
“Yanga ni bingwa wa kweli, tutathibitisha uwanjani kwamba tunastahili kubeba
tena taji la Ligi Kuu,” alisema Boniface Makunga, mwenyekiti
wa tawi la Yanga Manispaa ya Iringa.
Zaidi ya tambo na ushindani wa uwanjani, mashabiki hao walibainisha kuwa
tukio hilo litakuwa na manufaa ya kiuchumi kwa wakazi wa Iringa kupitia
biashara ndogondogo zitakazoibuka kutokana na ujio wa mashabiki kutoka ndani na
nje ya mkoa.
No comments:
Post a Comment