Kilolo, Iringa – Septemba 14,
2025
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa
(MCC) na Mratibu wa Kampeni Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Salim Abri maarufu
kama Asas, leo amezindua rasmi kampeni za Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kilolo
pamoja na wagombea wa nafasi za udiwani kupitia CCM katika jimbo hilo.
Mgombea Ubunge wa Kilolo, Dr.
Ritta Kabati, ndiye mwanamke pekee kati ya wagombea wa majimbo saba ya ubunge
mkoani Iringa kupitia CCM. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dr. Kabati
aliishukuru CCM kwa kuendelea kumuamini na kumpa jukumu la kupeperusha bendera
ya chama, akisisitiza kuwa uzoefu wake wa miaka 15 kama Mbunge wa Viti Maalum
umemwandaa vyema kuwatumikia wananchi wa Kilolo kwa bidii, uadilifu na upendo.
Ameahidi kutekeleza kikamilifu Ilani
ya CCM 2025–2030 bila upendeleo, huku akihimiza mshikamano kati ya viongozi na
wananchi, kuvunja makundi ya kijamii na kisiasa, na kuharakisha maendeleo ya
jimbo hilo. Aliwaomba wananchi kumpigia kura yeye, Rais Samia Suluhu Hassan na
madiwani wote wa CCM.
Kwa upande wake, Salim Abri
(Asas) alisema Dr. Kabati si mgeni katika uongozi, akibainisha kuwa Kilolo
imepata mgombea mwanamke mwenye maono, uzoefu na uwezo wa kushughulikia
changamoto za wananchi. Alisisitiza kuwa Dr. Kabati amejikita katika kupigania
huduma bora za afya, upatikanaji wa maji, kupambana na rushwa, na kusaidia
makundi maalum kama watu wenye ulemavu.
Aidha, Abri alitaja baadhi ya
mafanikio yaliyopatikana Kilolo chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, yakiwemo
ujenzi wa vituo vya afya vitano, zahanati kumi, vyumba vya madarasa 493, vyoo
352, miradi ya maji safi, pamoja na shule ya sekondari ya wasichana ya mkoa.
Alisema mafanikio hayo ni ushahidi wa utekelezaji bora wa ilani ya CCM
unaoendelea kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya
Kilolo, John Kiteve, alisema wananchi wa Kilolo wako tayari kuiunga mkono CCM
kwa kura zote, akibainisha kuwa ilani ya mwaka 2020–2025 imetekelezwa kwa
mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali, huku ilani ya 2025–2030 ikilenga
zaidi kutatua changamoto za wananchi na kuboresha maisha yao.
No comments:
Post a Comment