Monday, 18 July 2011
LUDEWA WAGOMA KUWAPOKEA WATANZANIA WAPYA
WANANCHI katika Wilaya ya Ludewa Mkoani Iringa, wamekataa katu kuwapokea wakimbizi kutoka Somalia na Ethiopia waliobatizwa kwa jina la watanzania wapya kwa madai kuwa watasababisha hasara kubwa kuliko faida imefahamika.
Mgomo huo umetokea jana katika kikao cha Baraza la Madiwani ambao ni wawakilishi wa wananchi kilichofanyika Julai 15 mwaka huu ambacho pamoja na mambo mengine kilihusisha bajeti ya mwaka ujao wa fedha na kuangalia hali halisi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha uliopita.
Awali akitoa taarifa ya kutaka ufafanuzi Diwani wa Kata ya Mawengi, Bw. Leodgar Mpambalyoto alisema kuna jambo lililoko mbele yetu linalowasumbua wananchi wengi ambalo ni agizo la serikali la kuwapokea watanzania wapya ambao wamebatizwa jina hilo kutokana na kuingia nchini na kupokelewa kama wakimbizi.
Kwa upande, wake Mpambalyoto aliishauri serikali kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi na baadhi ya wadau wakiwemo madiwani. “Ni wajibu wa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri kupokea maelekezo kutoka Serikali Kuu, lakini baraza lina uwezo wa kukataa au kukubali kwani ndiyo wawakilishi wa wananchi,” zoezi la kuwapokea watanzania wapya bila maelekezo litakuwa na athari kubwa sana tunaomba lisipuuzwe,” aliongeza.
Akichangia hoja hiyo Mbunge wa Ludewa Bw. Deogratius Haule Filikunjombe alisema kuwa waraka huu ulishasainiwa na rais tayari na ulishapitishwa, lakini ukiangalia zaidi watu hawa wakija wanamadhara zaidi kuliko faida.
“Pamoja na kwamba rais ameridhia mila za watu hawa na zetu hazifanani, wanakotoka ni watu wa vita, leo hii Ludewa tunaletewa watu elfu tatu je, wana Ludewa wameandaliwa? Sisi tupo tayari? Kama sehemu nyingine wanawahitaji, sisi Ludewa hatuwataki,”alisisitiza mbunge huyo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ludewa Bi. Hilda Lauwo aliwaambia madiwani hao kuwa anataarifa kuwa wahusika walisema wangekuja kutoa mafunzo hayo ili kupata uelewa aliwataka wasikatae mafunzo hayo na kwamba wayapate kwanza ndipo wayakatae.
Baadhi ya wajumbe waliohudhuria baraza hilo walishtushwa na hatua ya serikali kuleta wageni nyumbani kwao bila kuwashirikisha na kukubaliana, walisema pamoja na kwamba waraka huu umetoka kwa mkuu wa nchi ambaye ni Rais Jakaya Kikwete, siyo vizuri kuwaleta watu hawa wanaotoka kwenye vita katika maeneo yetu hatuwezi kujua wamekuja na nini.
“Sisi wenyewe hatuna sehemu ya kulima tunahangaika kwa umaskini sasa hawa watanzania wapya wanaotaka kuja katika miji yetu, kwani huko kwao walikotoka hawawezi kurudishwa?” waliuliza wajumbe hao kwa maskitiko.
Taarifa hiyo ya utengamanishaji wa mkakati wa kufungua makazi mapya na kuwezesha ukaaji wa watanzania wapya waliopewa uraia katika maeneo tofauti nchini, inasema serikali ya Tanzania kuwezesha uhamiaji wa makazi ya kaya za Watanzania wapya waliopewa uraia zipatazo 35,500 kutoka katika makazi ya wakimbizi.
Katika zoezi hilo serikali imeteua wilaya zaidi ya 50 kutoka mikoa 16 ambayo ni pamoja na Iringa kaya
3,000, Rukwa 3,000, Dodoma 3,500, Ruvuma 3,000, Shinyanga 1,600, Morogoro 1,600, Tabora 1,600, Tanga 1,600, Kigoma 1,000, Singida 1,600, Pwani 2,000, Mtwara 3,500, Mbeya 1,500, Manyara 1,500, Lindi 3,500, na Kagera 1,500 vigezo vilivyotumika katika uteuzi wa mikoa hiyo ni upatikanaji wa ardhi ya kulima na hali ya msongamano wa watu.
Wilaya ya Ludewa inazo tarafa tano, kata ishirini na tano na vijiji sabini na sita wakazi wake wako laki moja na nusu kwa mujibu wa Sense ya Mwaka 2000. Ludewa inavivutio vingi ikiwemo milima ya Livingstone, samaki wa mapambo Ziwa Nyasa, madini aina nyingi tofauti.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...
Na Friday Simbaya, Mufindi Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...
-
KIKUNDI cha Upendo ni kikundi cha kina mama 20 walioamua kujiunga kwa pamoja na kuanz...
-
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini MIEMBE hulimwa karibu katika nchi zote zilizoko kwenye ukanda wa joto, na hasa tropiki. Nchini ...
-
The most deadly form of tuberculosis is one that lies in wait inside the body for years, attacking at the first sign of weakness. Abou...
No comments:
Post a Comment