Na Friday Simbaya, Ludewa
WANANCHI wa Ludewa Mjini Makao Makuu ya Wilaya ya Ludewa mkoani Iringa wamesema kuwa hawaoni umuhimu wa kuwa na mamlaka ya maji mjini yaani ‘Ludewa Water Supply and Sanitation Authority (LUDSSA) kwa sababu tatizo la maji kwao linazidikuongeka kila kukicha huku mabomba yakitiririsha maji mitaani ovyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema Serikali ya Wilaya ya Ludewa haioni haja ya kusumbua vichwa kwa ajili ya kuondoa kero ya maji kwa sababu katika nyumba zao maji yamejaa mpaka wanashindwa kwa kuyapeleka kwani mwenye shibe hamjali mwenye njaa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Ludewa mjini, Bw Omary John Kiowi alisema kuwa wananchi wanayo haki ya kulalamika kwani kero hii ni aibu kwa wataalam wetu ambao miaka nenda rudi wanatoa sababu kuwa maji hayatoshi kwenye matanki huku waamebweteka bila kutafuta njia mbadala kuikabili hali hiyo.
Bw Benito Mgimba makazi wa Mtaa wa Kanisa B aliliambia Nipashe kuwa sasa ni miaka zaidi ya kumi maji katika mtaa wao ni ndoto hivi hata watoto wanaozaliwa wakiyaona mabomba katika mitaa mingine wanashangaa na kuogopa kwa sababu ni vitu vigeni kwao.
“Miaka miwili iliyopita tuliambiwa tuchimbe mitaro kwa nguvu zetu wenyewe ili tuletewe maji mtaani kwetu, lakini hadi leo hakuna kinachoendelea mitaro tumechimba bure na maji hayaletwi na hakuna taarifa yoyote, sisi hatuna kwa kwenda kulalamikia wanyonge,”alilalamika Benito.
Oscar Chaula na Romward Kiowi kwa upande wao walisema watendaji katika idara husika wameshindwa kuwajibika. “Katika mtaa wetu wa kanisa tuliweka bomba la kwanza wakasema ni dogo tukachanga fedha na kununua lingine kubwa, ni mwaka wa ishirini sasa tunakunywa maji yanayotumiwa na wanyama kama nguruwe, ng’ombe na punda kwenye madimbwi,” alisema Chaula.
Romwardi Kiowi alilalamika kuwa ni miaka mitatu tangu wachimbe mifereji kwa nia ya kutandaza mabomba, lakini hakuna kinachoendelea na kwaamba ni zaidi ya miaka zaidi ya mitano hajaona maji ya bomba, ila anashuhudia watoto wakiugua magonjwa ya matumbo kwa kunywa maji yasiyo salama kutoka kwenye madimbwi huku watendaji wakisubiri mishahara na kunywa pombe tangu asubuhi.
Cathbert Haule mkazi wa Mtaa wa Kanisa, Castory Mwachiro wa Mtaa wa Kanisa B, Tiemo Kayanda, Stephano Mahundi mkazi wa Mtaa wa Mkondachi, Valentina Mgeni, Lucy Haule wameilaumu serikali ya wilaya kwa kutoshughulikia kero ya maji ambayo ni muhimu sana kwa matumizi ya binadamu.
“Inashangaza na haiingii akilini wanaposema maji hayatoshi wakati mitaani maji yanamwagika ovyo, hakuna usimamizi wala uwajibikaji, mkurugenzi na watendaji wake tunataka huduma ya maji inawezekana vyanzo havitoshi, lakini tuyadhibiti haya yaliyopo watendaji acheni kushinda maofisini.””alilalamika Bw. Haule.
Akijibu malalamiko hayo Meneja wa Mamlaka ya maji mjini Ludewa (LUDWSSA), Bw. Atanasio Munge alikiri kuwapo kwa tatizo la maji katika baadhi ya maeneo ya mji wa Ludewa kama mtaa wa Kanisa B, miundombinu yaani mabomba yamechakaa, lakini pia bomba linalotoa maji kwenye Tanki na kuleta mjini ni dogo sana lina ukubwa wa 3 inch tu, wakati linachukua maji katika matanki mawili.
Bw. Munge alisema kutokana na tatizo hilo watu wanaopata maji tena ya mgao ni 65% ya wakazi wote wa Ludewa na kwamba hao wanalazimika kupata mara tatu kwa wiki na kuongeza kuwa mbali na uchakavu wa mabomba ongezeko la watu ni kubwa sana linafanya maji kuwa machache.
Hata hivyo, alitoa matumaini kwa wakazi wa Ludewa kwamba mamlaka ya maji ina mipango kabambe ya muda mfupi na mrefu katika kukabiliana na kero ya maji mjini kwa kupima na kusanifu chanzo cha maji cha Mapetu pamoja na kile cha Mwangacha ili kuhakikisha mitaa ya kanisa na kwingineko maji yanapatikana kwa uhakika.
Munge aliutaja mpango wa muda mrefu kuwa ni Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Maalum kwa Kata ya Ludewa mradi ambao utasimamiwa na mamlaka ya maji Ludewa (DED) na Msimamizi wa maji kutoka Mamlaka ya Maji Iringa Manispaa (IRUWASA) na tayari mzabuni Don Consultant ameshaanza kwa hatua ya kwanza ya vitabu vya zabuni na kwamba matanki mawili yenye ujazo wa m.300 yatajengwa Ludewa (K) na tanki moja lenye ujazo wa m.1000 litajengwa Ludewa (M) eneo la Kilimahewa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...
Na Friday Simbaya, Mufindi Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...
-
KIKUNDI cha Upendo ni kikundi cha kina mama 20 walioamua kujiunga kwa pamoja na kuanz...
-
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini MIEMBE hulimwa karibu katika nchi zote zilizoko kwenye ukanda wa joto, na hasa tropiki. Nchini ...
-
The most deadly form of tuberculosis is one that lies in wait inside the body for years, attacking at the first sign of weakness. Abou...
No comments:
Post a Comment