Monday, 6 October 2014

ITUNUNDU FC MABINGWA WA KOMBE LA SPANEST



Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba akimkabidhi kombe la ushindi wa ligi ya SPANEST, kapteni wa Itunundu Fc
Hapa akikabidhi cheti cha ushindi
Akiwavisha Itunundu FC medali za dhahabu
Akiwapa zawadi ya mpira miwili
Itunundu FC katika shamrashamra
Kapteni wa Kinyika FC akipokea zawadi ya mpira, cheti na Sh 200,000 taslimu
Alipokuwa akikagua timu
Timu zikionesha nembo ya ligi hiyo
KLABU ya Itunundu (Itunundu FC) imetwaa kombe la SPANEST, kitita cha Sh300,000, seti moja ya jezi, mpira mmoja, medali za dhahabu na cheti baada ya kuibwagwa kwa bao 1-0 Kinyika FC katika fainali za ligi hiyo zilizopigwa juzi kwenye uwanja wa Kimande Pawaga, Iringa Vijijini.
Kwa ushindi wa fainali ya ligi hiyo yenye kauli mbiu “Piga Vita Ujangili, Piga Mpira Okoa Tembo” inayolenga kuongeza mwitikio wa vijana katika harakati za serikali na wadau wake za kupambana na ujangili, Itunundu FC imepewa pia fursa ya kutembelea bure Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Bao hilo lililoizamisha Kinyika FC iliyoonekana kuutawala mchezo kwa karibu dakika zote za mchezo liliwekwa kimiani na mshambuliaji wa kati wa Itunundu FC, Siani Chambulika katika dk 39 ya kipindi cha kwanza.
Chambulika (18) alionekana shujaa mbele ya mashabiki zaidi ya 5,000 wa tarafa ya Idodi na Pawaga waliohudhuria fainali hiyo ya kwanza ya kombe hilo baada ya kupokea pasi kutoka kwa kiungo mshambuliaji Klopa Mtogesewa na kufanikiwa kuwaadaa walinzi wa Kinyika FC kabla ya kuachia shuti kali lililomshinda golikika wa Kinyika FC, Asid Samre na kuzama kimiani.
Pamoja na Kinyika FC kufanya mabadiliko matatu katika kipindi cha pili kwa kuwatoa Elisha Sila, Ramadhani Kapova na Jeremia Manga na kuwaingiza Robert Mahombero, Myagaro Mwiravi na Festo Savya, hawakufanikiwa kupenya ngome ya Itunundu FC.
Pamoja na kupoteza mchezo huo uliohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba, Mwakilishi wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Elliud Mvella, madiwani, makaribu tarafa ya Idodi na Pawaga na wawakilishi wa SPANEST na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Kinyika FC waliondoka na Sh200,000, cheti, medali za shaba, mpira mmoja na seti moja ya jezi.
Mshindi wa tatu, Kitisi FC alijinyakulia cheti na Sh 100,000 baada ya kuibwaga Kimande FC kwa bao 1-0. Zawadi zote kwa washindi zilikabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma.
Ligi hiyo itakayokuwa ikichezwa kila mwaka inashirikisha vijiji 21 vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Tarafa ya Idodi na Pawaga (Mbomipa) inayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo sehemu yake kubwa ipo wilayani Iringa.

Wapenzi wa soka watakaopenda kujumuika na timu Itunundu FC kujionea rasilimali mbalimali zilizoko katika hifadhi ya Ruaha, kwa mujibu wa Mratibu wa Spanest ambao ni Mradi wa Kuboresha Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Godwell Ole Meing’ataki watalazimika kuchangia Sh 25,000 kwa ajili ya usafiri wa kwenda na kurudi pamoja, chakula na tozo la kuingia katika hifadhi hiyo. (BONGOLEAKS)

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...