Moshi/Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa
wa Kilimanjaro, jana imemhukumu raia wa Pakistan Ahmed Kamran kifungo
cha miaka 60 jela baada ya kumtia hatiani kwa makosa manne ikiwamo
kusafirisha twiga wanne hai kwenda Qatar.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mfawidhi wa
mahakama hiyo, Simon Kobelo, ambaye pia aliamuru kutaifishwa kwa mali
zote za mtuhumiwa huyo zilizopo katika ardhi ya Tanzania.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana baada ya
kutolewa hukumu hiyo, Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji
Peter Msigwa alisema kilichofanyika ni kutaka kuonyesha haki imetendeka,
huku Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira,
James Lembeli akisema kuwa kumsaka mtuhumiwa huyo ni sawa na mchezo wa
kuigiza.
Hata hivyo, tayari Shirika la Polisi la Kimataifa
(Interpol) juzi limewataka Watanzania kusaidia katika kumsaka Kamrani,
huku likitangaza kuanzisha operesheni iliyoipa jina la Infra Terra
ikilenga kuwanasa watuhumiwa uharamia zaidi ya 139 katika nchi 36
duniani.
Mchungaji Msigwa alisema kuwa kilichofanyika ni
kiini macho kwa kutaka kuonyesha kuwa haki imetendeka. Alisema
haiwezekani Ahmed apatikane na kosa pekee yake wakati mchakato wa
kusafirisha wanyama unaonyesha watu wengi wakiwamo viongozi walishiriki
kutekeleza biashara hiyo.
“Hata kama wangemfunga miaka 200 haisaidii kitu,
hapo mahakama imefanya kazi yake lakini Serikali inafanya kiini macho,”
alisema Msigwa.
Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini,
alisema kitendo cha mahakama kuthibitisha kuwa mfanyabiashara huyo
alikuwa na vibali halali kinaonyesha kuwa kuna baadhi ya watu
walishiriki kumtorosha ili wasitiwe nguvuni.
“Isingewezekana ndege iingie nchini bila wakubwa kujua ilikuja kufanya nini?” alihoji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili
na Mazingira, James Lembeli alisema kumsaka mtuhumiwa Kamran Ahmed
anaona huo ni mchezo kwa sababu mtuhumiwa huyo raia wa Pakistan
alishatoroka awali kisha akapatikana, lakini katika hali ya kushangaza
akapewa tena dhamana.
Lembeli alisema hatua ya kuruhusu dhamana ya pili
kwa mtuhumiwa huyo inatia shaka kuwa kuna jambo lisilo la kawaida
lililomwezesha kutoroka kwake.
“Hivi kwa nini walimpa dhamana wakati alishatoroka
mara ya kwanza na huyu mwandishi Temba aliyemdhamini sijui alianzia
wapi, najua hamfahamu lakini amejiingiza kwenye matatizo ya kujitakia,”
alisema Lembeli.
Kuhusu ndege inayodaiwa kutumika kusafirisha
wanyama hao, ambapo mahakama imethibitisha kuwa ilikuwa na vibali vyote
halali vya kuingia nchini kwa safari ya kidiplomasia, Lembeli alisema
Wizara ya Mambo ya Nje ieleze kwa kina jambo hilo lilitokeaje.
No comments:
Post a Comment