Basi la kampuni ya Enuel lenye namba za usajili T 919 DCD kulia likiwa limegongana na lori usajili T 122 ALW mali ya Trasisco ya mkoani Arusha
|
WATU wanne wamefariki dunia papo hapo na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa vibaya baada ya basi la kampuni ya Enuel Express kugongana na lori eneo la kijiji cha Idetero wilaya ya Mufindi mkoani Iringa .
Ajali hiyo imetoka asubuhi ya leo wakati basi hilo likitokea Mbeya kuelekea Dodoma huku mashuhuda wa ajali hiyo wakidai kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi hilo ambae alitaka kuyapita magari mawili yaliyokuwa mbele yake pasipo kuchukua tahadhari .
Farida John ambae ni mmoja kati ya abiria waliokuwepo katika basi hilo alisema kuwa eneo hilo ambalo ajali imetokea ni eneo ambalo lina mlima mkali na kuwa dereva wa basi hilo alikuwa akishuka na Lori likipandisha mlima huo na kuwa mbele kulikuwa na basi na lori bovu hivyo dereva wa basi hilo kuona hivyo alizimika kulitoa basi hilo nje ya barabara ndipo walipogongana na lori hilo.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Ramadhan Mungi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo mbaya na kuwa basi hilo lenye namba za usajili T 919 ACD liligongana na lori lenye namba za usajili T 122 ALW mali ya Trasisco ya mkoani Arusha likiwa na tela namba T 203 ATS ambalo lilikuwa likitokea Mafinga kuelekea Makambako mkoani Njombe.
Alisema kuwa mbele ya basi hilo lililipata ajali kulikuwa na basi jingine ambalo liliongozana yote yakielekea Iringa na baada ya kufika eneo hilo la ajali kulikuwa na lori bovu lenye namba T 647 ABK likiwa na tela lenye namba T 388 AYF lililokuwa limeharibika eneo hilo na kupelekea basi la mbele kusimama nyuma ya lori hilo huku basi hilo likijaribu kutaka kulipita lori hilo .
" Wakati dereva wa lori hilo akijaribu kulipita lori hilo na basi ghafla mbele yake aliona lori ambalo lilikuwa likija mbele yake hivyo katika kuepusha kugongana uso kwa uso ..... dereva wa basi aliamua kulitoa basi lake nje ya barabara upande wa kulia na dereva wa lori ambalo lilikuwa likija mbele yake nae aliamua kulitoa lori hilo nje ya barabara kushoto na ndipo walipogongana nje ya barabara baada ya wote kukwepana kugongana uso kwa uso na kugongana nje ya barabara "
Kamanda Mungi alisema katika ajali hiyo abiria wawili waliokuwa katika basi hilo walikufa papo hapo na wengine ambao idadi yao bado kufahamika walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospital ya Mafinga wilayani Mufindi na baadhi yao kukimbizwa Hospital ya Makambako .
Hata hivyo alisema kuwa katika lori hilo hadi majira ya saa 8 mchana jitihada za kuitoa miili ya watu wawili ambao vichwa vyao vilikuwa vikionekana ilikuwa ikiendelea japo idadi kamili ya watu waliokuwemo katika lori hilo bado haijafahamika zaidi ya watu miili hiyo miwili ambayo vichwa vilikuwa vikionekana.
Hata hivyo alisema taarifa kamili na idadi kamili ya waliokufa na majina yao itatolewa mara baada ya zoezi la kuitoa miili ya watu hao iliyobanwa katika lori hilo kukamilika. (imehaririwa na Friday Simbaya)
No comments:
Post a Comment