Monday, 27 April 2015

WANAWAKE 512 WAGUNDULIKA NA KANSA YA SHINGO YA KIZAZI

MKOA wa Iringa umeweza kuchunguza kina mama 11,223 na kati hawa wanawake 512, (sawa na asilimia 4.6) waligundulika kuwa na mabadiliko ya awali na kupewa tiba katika kipindi cha kuanzia Januari 2014 mpaka Januari 2015.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi, Mkoa wa Iringa, Adam Swai wakati wa mkutano wa kufunga na kutoa tathmini ya mradi wa kuhamasisha jamii kuhusu huduma za uchunguzi wa saratani ya mlango wa shingo ya kizazi.

Alisema kuwa haya ni mafanikio makubwa yanayohitaji kuendelezwa na kuongeza kuwa wanawake 6,322, sawa na asilimia 56 walichunguzwa kwa jihudi za Shirika la Bristol Myers Squibb Foundation (BMSF) kupitia Taasisi ya T-MARC Tanzania.

Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huu hapa Iringa, walengwa wakuu wa mradi walikuwa ni wanawake wenye umri wa miaka 30 hadi 50 katika maeneo ambayo wanajamii wako hatarini kupata saratani ya mlango wa kizazi kutokana kiwango cha maambukizi ya VVU kuwa juu.

“Walengwa wengine walikiwa makundi yote yenye ushawishi kwa walengwa wakuu katika uchunguzi wa afya zao, ili wawahamisishe kufanya maamuzi wa kupata huduma za uchunguzi na matibabu. Wanaume pia walishirikishwa katika mradi huu,” alisema Swai.

Alisema kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazokumbwa na tatizo kubwa la saratani ya mlango wa kizazi duniani.

Asilimia 25 ya wanawake wa Tanzania wako hatarini kupata saratani ya mlango wa kizazi katika maisha yao, na saratani ya mlango wa kizazi ni mojawapo ya sababu zinazosababisha vifo vya wanawake nchini, alisema.

Takiwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inaonyesha katika wa wagonjwa wa saratani wanaopekwa katika taasisi hiyo kila mwaka, zaidi ya wagonjwa 5,000 wanatatizo la saratani ya mlango wa kizazi. 

Wataalamu wa mambo ya saratani wamegundua kuwa kuna uwiano mkubwa kati ya saratani ya mlango wa kizazi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Takimwi za utafiti wa viashiria vya UKIMWI na Malaria nchini zinanaonesha kuwa Mkoa wa Iringa ni wa pili nchini kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU.

Haya hivyo, katibu tawala msaidizi huyo alisema kuwa serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inafanya juhudi mbalimbali katika kupambana na saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake.

“Hii ni kwa sababu saratani ya mlango wa kizazi inatibika. Ila tu ili iweze kutibika, ni muhimu kuwa saratani hii igundulike katika hatua zake za awali, ” alisisitiza Swai.

Kwa upande wake, Meneja Ufualiaji, Tathmini na Utafiti kutoka T-MARC Tanzania, Dkt. Benjamin Kamala alisema kuwa mradi huu ulifadhiliwa na Shirika la Bristo Myers Squibb Foundation (BMSF) kupitia Pink Ribbon Red Ribbon (PRRR); ulitekelezwa nchini Tanzania kwa ushirikiano na mashirika matano ambayo ni T-MARC Tanzania, Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA), Asasi ya Tanzania Youth Alliance (TAYOA) na mtandao wa wadau wa UKIMWI Mbeya (MHNT).



Alisema kuwa mradi pia ulihusisha vituo mbalimbali vya afya ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Iringa, Hospitali ya Lugoda, Kituo cha afya Ipogolo, Hospitali ya Tosamaganga, Kituo cha afya Marie Stopes, Hospitali ya Mafinga, Kituo cha afya Usokami na Hospitali ya Ilula.



“Huu ni mwendolezo wa juhudi za wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake wa Tanzania,” alisema Dkt Benjamin.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...