Siku moja baada ya taasisi ya Twaweza kutangaza ushindi mnono kwa mgombea Urais wa CCM, Dk John Pombe Magufuli dhidi ya Mgombea Urais wa Ukawa Edward Lowassa, Kada wa chama cha Mapinduzi Januari Makamba amepinga matokeo hayo akidai wamepunguziwa ushindi.
Makamba amesema kwamba utafiti huo umewapunguzia ushindi chama cha Mapinduzi kwa kuwa katika utafiti wao ulionesha Magufuli angeshinda kwa asilimia 69 dhidi ya asilimia 65 ya Twaweza.
Akizungumza na moja ya gazeti hapa nchini Makamba amesema CCM haistushwi na utafiti huo kwa mgombea wao amefika maeneo mengi nchini Tanzania kufanya mikutano.
Akitangaza matokeo hayo mkurugenzi wa TWAWEZA Aidan Eyakuze, amesema utafiti huo ulifanyika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, na ulifanyika kwa njia ya simu kukusanya maoni ya wananchi katika mikoa yote ya Tanzania.
Eyakuze amesema kuwa wananchi waliulizwa swali kuwa watamchagua nani bila kutajiwa majina na walipoombwa kutaja moja kwa moja jina la mgombea Urais ambaye wangemchagua, asilimia 65 ya wananchi walimtaja mgombea wa CCM Dkt. John Magufuli.
Amesema asilimia 25 walimtaja mgombea wa Chadema kupitia Ukawa, Edward Lowassa, asilimia 10 iliyosalia iligawanyika kati ya wale waliomtaja mmoja miongoni mwa wagombea urais wengine, waliokataa kujibu na waliokuwa bado hawana mgombea waliyempendelea.
Katika hatua nyingine wasomi mbalimbali wamepinga utafiti huo akiwemo Mkurugenzi wa tasisi ya SIKIKA Inei Kiria akidai kuwa idadi ya wapiga kura katika utafiti huo haitoshi kuwakilisha idadi ya wapiga kura milioni 24 nchi nzima.
No comments:
Post a Comment