Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amani Juma Masenza akiongea na wananchi wa Mkoa wa Iringa kupitia vyombo vya habari kwa kuwatakia heri katika sherehe za Noeli na Mwaka Mpya 2017 leo ofisini kwake. (Picha na Friday Simbaya)
IRINGA: Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amekemea vitendo vya ubakaji na ulawiti vinavyoendelea kujitokeza katika jamii na kuonya kwamba vitendo hivyo visitokee tena mwaka 2017.
Mkuu mkoa huyo alisema hayo leo (Jumatatu) wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo alitumia pia fursa ya kuwatakia wananchi wa Mkoa wa Iringa heri katika Noeli na Mwaka Mpya 2017.
Masenza ameviagiza vyombo vya dola vifanye kazi ya kuwabaini wahusika na kuwafikisha kwenye mkondo wa sheria.
Pia, mkuu huyo aliwaomba wananchi wa Mkoa wa Iringa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ubakaji kwa watoto wadogo.
“Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunatokomeza kabisa vitendo vyote vinavyopelekea uvunjifu wa amani katika mkoa wetu wa Iringa na nchi kwa ujumla,” alisema Masenza.
Aidha, mkuu huyo aliwaomba wananchi wa Mkoa wa Iringa kwa umoja wahakikishe wanasimamia na kudumisha ulinzi na usalama ili mkoa uendelee kuwa na amani na utulivu.
“Napenda kuwatakia sikukuu njema ya Noeli na Mwaka Mpya 2017 wenye mafanikio tele. Ninawasihi kuhakikisha mnasherehekea sikukuu hizi kwa amani, usalama na utulivu,” alisema.
Alisema kuwa serikali itahakikisha ulinzi na usalama vinakuwepo kipindi chote cha sikukuu kwa sababu uzoefu unaonesha kuwa katika majira ya sikukuu watu wasiopenda kuona amani na utulivu wa mkoa hutumia majira haya kufanya uhalifu.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza ni wa 21, tangu kuanzishwa kwa mkoa huu mwaka 1964, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Iringa alikuwa Philemon Muro (1964-1968).
Wakati huohuo, mkuu wa mkoa ametoa wito kwa wananchi kutumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha kwa kuhakikisha wanapanda mazao ili kujihakiishia uhakika wa chakula.
Alisema kuwa katika maeneo yanayopata mvua chache hususan Mahenge na Isimani wapande mazao yanayovumilia ukame.
Aidha, mkuu wa mkoa huyo aliwakumbusha wananchi kupanda miti katika msimu huu wa mvua kwa kuwa mkoa una hali ya hewa nzuri inayostawisha miti.
No comments:
Post a Comment